Gamondi: Nina timu bora, imekamilika
MICHEZO
Published on 24/08/2024

KOCHA Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi anajivunia kikosi chake akisema ana timu iliyokamilika kila idara.

Gamondi amejivunia hayo leo Agosti 23 wakati wa mkutano wa na waandishi wa habari Makao Mkuu ya Yanga, Dar es Salaam kuelekea mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O Agosti 24.

Katika mchezo wa kwanza Yanga ilishinda kwa mabao 4-0.

Kikosi rasmi cha wachezaji na benchi la ufundi la Yanga msimu 2024/2025

“Nina timu bora ambayo imekamilika kila idara. Kwenye mpira lazima uwe na weledi kwa kuheshimu wapinzani,” amesema Gamondi.

SOMA: Yanga yapewa Vital’O, Azam kuivaa APR

Amesema hawezi kusema kuwa Yanga haiwezi kufungwa goli tano, lakini sio jambo analokitarajia kuliona likitokea na kwamba anafahamu Vital’O itakuja kwa nguvu kutafuta magoli lakini timu yake imejiandaa kwa kila mbinu.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

Gamondi ameongeza: “Tunajiamini na matokeo tuliyopata mechi iliyopita lakini bado tunaheshimu kuwa tuna dakika 90 nyingine za kupambana, kipaumbele chetu ni kufuzu hatua inayofuata.”

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake golikipa Aboutwaleeb Mshery amesema hawafikirii mechi iliyopita, ila mchezo ujao ni kama wanaanza upya bila kujali yaliyotokea.

Golikipa wa Yanga, Aboutwaleeb Mshery.

“Tunayo hamasa kubwa kuhakikisha kuwa tunashinda mchezo unaokuja. Kiukweli tunaitamani sana hela ya Mama (Rais Samia), hivyo tunakwenda kujitolea kwa kiwango kikubwa,” amesema Mshery.

Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema anashangaa kusikia watu wanasema Clement Mzize inabidi atoke ili akakue zaidi, lakini watu hao hao hawaangalii klabu hiyo ilipomtoa ila bado yupo sana Yanga na kwamba wananchi wapuuze maneno yao kwani lengo lao ni kuivuruga timu hiyo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe.

“Kama ndoto zenu ni Mzize aondoke kwa sababu ambazo hazina kichwa wala miguu, chini ya Injinia Hersi hawezi kuondoka Yanga,” amefafanua Kamwe

Yanga inahtaji sare yoyote au kufungwa si zaidi ya mabao 4 na Vital’O ya Burundi kujihakikishia kucheza hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Comments
Comment sent successfully!