Mashambulio mabaya ya anga ya Israel na shambulio la Hezbollah yameibua hofu kwamba huenda usitishaji mapigano nchini Lebanon ukasambaratika.
Watu kumi wameuawa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatatu usiku, wizara ya afya imesema, baada ya Israel kufanya mashambulio makubwa zaidi ya anga tangu pande zote mbili zilikubali wiki iliyopita kumaliza mzozo wa miezi 13.
Jeshi la Israel lilisema liliwashambulia wapiganaji wa Hezbollah, maeneo ya kurushia makombora na miundombinu na kuitaka serikali ya Lebanon kuzuia kile ilichokiita "shughuli za uhasama" za kundi hilo.
Hezbollah imerusha makombora mawili kwenye kambi ya jeshi la Israel katika eneo la mpakani linalozozaniwa, ikisema ni onyo juu ya kile ilichokiona kama "ukiukaji wa mara kwa mara" wa mapatano kwa upande wa Israel. Hakuna majeruhi walioripotiwa.
Marekani, ambayo pamoja na Ufaransa ilipitisha makubaliano hayo na inafuatili, inasema "kwa kiasi kikubwa" usitishaji mapigano ulikuwa ukiendelea licha ya ghasia.
Mzozo huo ulianza tarehe 8 Oktoba 2023, pale Hezbollah iliporusha makombora kaskazini mwa Israel kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza siku moja baada ya shambulio baya la mshirika wake Hamas katika eneo la kusini mwa Israel.
Israel ilianzisha mashambulizi makali ya anga na uvamizi wa ardhini dhidi ya kundi hilo. Mamlaka za Lebanon zinasema zaidi ya watu 3,960 waliuawa, wengi wao wakiwa raia.
Mamlaka ya Israel inasema zaidi ya wanajeshi 80 wa Israel na raia 47 waliuawa.