Wamiliki wa jengo la Kariokoo washtakiwa kwa mauaji ya kutokusudia
HABARI
Published on 30/11/2024

Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.

Washtakiwa wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa jengo lililoporomoka katika makutano ya Mitaa ya Mchikichi na Kongo, Kariakoo, Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 29, walipandishwa kizimbani, Ijumaa, Novemba 29, 2024.

Washitakiwa hao waliotambuliwa kuwa Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach; Zenabu Islam (61), mkazi wa Kariakoo; na Ashour Awadh Ashour (38), mkazi wa Ilala.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Novemba 16, 2024 katika mitaa ya Mchikichi na Kongo, Kariakoo, Dar es Salaam, kinyume cha sheria na kwa pamoja walishindwa kutimiza wajibu wao na kusababisha vifo vya watu 29.

Akitembelea eneo la Kariakoo mara baada ya kuwasili kutoka kuhudhuria Mkutano wa Viongozi wa G20 mjini Rio de Janeiro, Brazil, Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia zoezi la kufanya usafi ambalo linaweza kufungua njia ya kubaini iwapo kuna watu wengi zaidi walionaswa katika eneo hilo.

Katika ziara yake katika eneo la tukio, Rais Hassan aliahidi kuwa uongozi wake utatekeleza kikamilifu mapendekezo ya kamati iliyoundwa hivi sasa kukagua hali na miundo ya majengo katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Rais Hassan alikuwa akizungumzia kamati aliyoiagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusimamia uundaji wa timu iliyopewa kazi ya kukagua kwa kina majengo yote ya Kariakoo ili kutathmini hali yake ya kimuundo.

 

Comments
Comment sent successfully!