Waokoaji wa Uhispania wako kwenye msako, kuwatafuta watu waliopotea kwenye gereji za chini ya ardhi na maegesho ya orofa kadhaa baada ya mafuriko makubwa ya wiki iliyopita huko Valencia.
Inahofiwa wanunuzi na wafanyakazi walinasa ndani ya maegesho ya magari katika duka moja huko Aldaia nje kidogo ya Valencia, maji ya mafuriko yalipopiga eneo hilo.
Polisi wamethibitisha kuwa hakuna waathiriwa waliopatikana katika magari 50 ya kwanza yaliyokaguliwa katika eneo hilo.
Lakini ripoti zinaonesha magari haya yalipatikana karibu na mlango wa maegesho ya magari, na magari mengine bado yamezama na bado hayajaopolewa.
Haya yanajiri wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Uhispania (AEMET) ikiweka sehemu ya eneo la kaskazini-mashariki la Catalonia kwenye tahadhari kutokana na mvua kubwa, huku mji mkuu wake Barcelona ukikumbwa na mafuriko Jumatatu asubuhi.
Vyombo vya habari vilionesha picha za magari yaliyozama kwa kiasi kwenye barabara kuu na maji ya mafuriko yakiingia kwenye basi.
Maji pia yameingia katika sehemu za uwanja wa ndege wa El Prat wa jiji hilo ikijumuisha eneo la umma la Terminal 1 na zaidi ya safari 60 za ndege zimeahirishwa au kucheleweshwa. Huduma za reli zimesitishwa