"Tuna mengi ya kujadiliana leo, na ninatazamia sana kushirikiana nanyi na kuendelea kuimarisha uhusiano wetu." Alisema von der Leyen akimkaribisha Starmer mjini Brussels.
Von der Leyen alisema kama washirika wenye mitizamo inayofanana, ni muhimu kushirikiana kwa karibu kwa kuzingatia mitizamo yao katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Starmer yuko mjini Brussels kwa ziara yake ya kwanza katika jitihada zake za kurejesha uhusiano na Umoja wa Ulaya, ambao ulikuwa wa mashaka na serikali iliyopita ya Conservative.
Kiongozi huyo wa chama cha Labour alisema alikuwa anataka Brexit iwe ya manufaa kwa Waingereza na kutuliza mahusiano na Umoja huo ili kuimarisha uchumi na maslahi ya usalama.