Kiongozi wa vuguvugu la kujitenga Cameroon akamatwa Norway
HABARI
Published on 26/09/2024

Kiongozi wa Cameroon anayetaka kujitenga amekamatwa nchini Norway kwa madai ya kuhusika katika mzozo wa silaha unaoendelea katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Lucas Ayaba Cho alikamatwa Jumanne kutokana na shutuma kuhusu " matamshi yake mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii", wakili wake aliiambia BBC.

Cho ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika vuguvugu la Anglophone (wazungumza kiingereza) linaloshinikiza uhuru kutoka kwa Cameroon, ambapo zaidi ya watu 6,000 wameuawa na wengine karibu milioni moja kuhama makazi yao tangu mapigano yalipoanza mnamo 2016.

Baadhi ya watu katika mikoa miwili ya nchi inayozungumza Kiingereza wanasema wanabaguliwa na watu wengi wanaozungumza Kifaransa.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeshutumu wanajeshi wa serikali na wale wanaojitenga kwa mauaji, ubakaji na mateso kwa raia.

Afisa mmoja wa Cameroon aliiambia BBC kwamba Norway na Cameroon walikuwa na makubaliano ya kiusalama, ambayo yanaweza kumfanya Cho arudishwe katika siku zijazo.

Tangu kuzuka kwa mzozo, serikali ya Cameroon imekuwa ikizitaka nchi za kigeni zinazowakaribisha viongozi wanaotaka kujitenga kuwarejesha nyumbani ili kujibu kesi zao kuhusu jukumu lao katika ghasia zinazoendelea

Comments