DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mtendaji wa Asasi za kiraia (FCS) Justice Rutenge amesema katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050 wananchi wanapaswa kupaza sauti zao kwa kutoa maoni yatakayopelekea kupata dira bora kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Rutenge amesema hayo leo Dar es Saalam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2024, itakayofanyika Septemba 9 hadi 13 Arusha ambapo zaidi ya washiriki 500 wanatarajiwa kushiriki na kutoa wito kwa watanzania kushiriki kwa wingi.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo ‘Sauti, Maono na Thamani’ lengo likiwa ni kutoa fursa zaidi kwa wananchi kupaza sauti zao kwa pamoja ili kurahisisha mchakato mzima wa upatikanaji wa dira hiyo.
SOMA: Dira ya Maendeleo 2050 kuwekeza rasilimaliwatu
Mkurugenzi mkazi, CBM International Nesia Mahenge amesema wiki hiyo inalenga kutatua changamoto ambazo zipo katika azaki za kiraia na kuona ni namna gani zinatatuliwa.
Mkurugenzi wa Ubongo international Mwasi Wilmore ambao watashiriki kwa kiasi kikubwa katika wiki hiyo amesema kwa niaba ya kampuni wanayofuraha kushiriki katika wiki hiyo kwa kuwa watapata mengi na kuonesha nini wanafanya ambayo yatakuwa na tija kwa jamii.