Polisi nchini Uganda imesema imewakamata watu 104 wakati wa maandamano ya kupinga ufisadi wiki hii.
Polisi imesema karibu wote waliokamatwa wameshtakiwa kwa makosa ya kuvuruga utulivu wa umma. Hii ni kwa mara ya kwanza polisi ya Uganda kutoa idadi ya waandamanaji waliokamatwa.
Marekani na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu, wamekosoa hatua za serikali za kuyazima maandamano hayo na kutaja wasiwasi wao wa kukamatwa kwa makumi ya watu ambao wamesema walikuwa wakiandamana kwa amani.
Vijana wa Uganda walifuata msukumo wa wenzao wa Kenya na waliingia mitaani Jumanne na Alhamisi kupinga ufisadi unaodaiwa kufanywa na viongozi waliochaguliwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.