Rais wa Cameroon yuko katika hali "nzuri", maafisa wakuu wamesisitiza baada ya kutokuwepo kwa muda mrefu kulilokozua uvumi ulioenea kuhusu hali ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 91.
Rais Paul Biya hajaonekana hadharani tangu tarehe 8 Septemba, alipohudhuria kongamano la China na Afrika mjini Beijing.
Tangu wakati huo amekosa matukio ambayo ilipangwa awepo, kama vile Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko New York.
Lakini katika taarifa yake, mkuu wa baraza la mawaziri la kiraia la Cameroon alisema Biya yuko vizuri na kulaani "watu waovu" wanaokisia kuhusu afya ya rais na "kifo".
Kauli hiyo imekuja baada ya siku kadhaa za vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia kutaka taarifa kuhusu afya ya Biya na mahali alipo.