Msukosuko wa upinzani Afrika Kusini baada ya makamu wa Malema kujiuzulu
News
Published on 24/08/2024

(L-R) Floyd Shivambu and Julius Malema at the Economic Freedom Fighters (EFF) election manifesto launch in Durban, South Africa - February 2024

Chanzo cha picha,Getty Images

Maelezo ya picha,Floyd Shivambu (kushoto) na Julius Malema katika uzinduzi wa ilani ya uchaguzi ya Economic Freedom Fighters (EFF) mjini Durban, Afrika Kusini - Februari 2024


  •  

Chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini, ambacho kimekuwepo kwenye siasa kwa zaidi ya muongo mmoja, kimepata pigo kufuatia kujitoa kwa naibu kiongozi wake Floyd Shivambu na kujiunga na chama cha Rais wa zamani Jacob Zuma - Umhkonto weSizwe (MK) au Mkuki wa Taifa.

Shivambu alionekana kama gwiji wa itikadi za EFF, huku kiongozi wa chama Julius Malema akijivisha vazi la kamanda mkuu - au "mpiga kelele-mkuu," kama wakosoaji wake wanavyomwita kutokana na maneno yake makali ya kutaka kutaifishwa kwa ardhi zinazomilikiwa na wazungu na migodi, na kuondoa ukoloni katika elimu.

Wawili hao walionekana kuwa timu yenye ushawishi, kwani EFF ilipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana wa Afrika Kusini, wanaokerwa na kasi ndogo ya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi tangu kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

Lakini EFF ilipata msukosuko mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Mei - haikufikia lengo lake la kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili – na badala yake imeshuka hadi nafasi ya nne.

MK imekuwa ndio adui wake wa kisiasa - kama ilivyo kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), kimepata kura kutoka kwa vyama vyote viwili na kunyakua nafasi ya tatu katika uchaguzi wa kwanza kushiriki.

"MK imepata kura kutoka kwa wafuasi wa ANC na EFF. Ilibadilisha mkondo wa siasa za Afrika Kusini, na kuifanya ANC kupoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza tangu 1994," anasema William Gumede, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Wits School of Governance huko Johannesburg.

 
Jacob Zuma and Julius Malema address the crowd gathered at a rally for the ANC Youth League's 66th anniversary at a stadium in Stellenbosch, South Africa - October 2010

Chanzo cha picha,Getty Images

Maelezo ya picha,Julius Malema (kulia) alikuwa mshirika wa Jacob Zuma (kushoto) na aliwahi kuongoza tawi la vijana la ANC.

Kuondoka Shivambu ni pigo kwa Malema, kwa sababu wawili hao, wakiwa vijana wenye nguvu za kisiasa, walianzisha EFF kwa pamoja wakati ANC, ikiongozwa na Zuma - ilipowafukuza.

Walifukuzwa baada ya shutuma za kuleta migawanyiko na kukiingiza chama katika mitafaruku.

"EFF ilichukua karibu vijana wote wa ANC, na pia kutawala siasa za wanafunzi katika vyuo vikuu kote Afrika Kusini, huo ndio ulikuwa mvuto wa chama miongoni mwa vijana," anasena Paddy Harper, mwandishi wa habari wa gazeti la Afrika Kusini la Mail & Guardian.

"Malema alikuwa na mvuto wa kupata uungwaji mkono, na Shivambu alikuwa na akili kutoa mwelekeo wa kiitikadi."

"Kwa kuachana kwao, EFF itaingia katika kipindi kigumu. Na hilo litaonekana kote Afrika Kusini, kuanzia vyuo vikuu hadi bungeni, huku EFF ikijaribu kuzuia kupoteza wafuasi zaidi kwenda MK."

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Moeletsi Mbeki anasema, kutengana huko kutaimarisha nafasi ya Malema katika chama, kwani hatakabiliwa tena na tishio kwa mamlaka yake.

"EFF inachukuliwa kama ni dhehebu linaloendeshwa na Malema. Katika mfumo kama huo, kiongozi ndiye kiongozi.”

Comments
Comment sent successfully!