Utawala wa kijeshi wa Niger wasitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine
News
Published on 08/08/2024

Niger imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine, hatua inayoashiria mgawanyiko unaoendelea kati ya Kyiv na baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi.

Serikali ya kijeshi ya Niger ilisema ilichukua hatua hiyo kwa "mshikamano" na nchi jirani ya Mali, ambayo ilikatiza uhusiano wake na Ukraine siku mbili zilizopita.

Nchi zote mbili zilichukizwa na matamshi ya afisa wa kijeshi wa Ukraine, ambaye aliashiria kuwa Kyiv ilihusika na mauaji ya makumi ya wanajeshi wa Mali mwezi uliopita.

Ukraine imekuwa ikijaribu kushinda washirika barani Afrika katika muda wote wa vita vyake na Urusi, yumkini katika jaribio la kukabiliana na ongezeko la ushawishi wa Moscow katika bara hilo.

Mwishoni mwa Julai, wanajeshi wengi wa Mali, pamoja na mamluki wa kundi la Wagner la Urusi, waliuawa katika mapigano na waasi wanaotaka kujitenga na wenye mafungamano na al-Qaeda.

Utawala wa kijeshi wa Mali uligeukia kundi maarufu la Wagner mnamo 2021, kuwasaidia kushughulikia maswala ya ukosefu wa usalama.

Baada ya Wagner kuthibitisha "hasara" katika shambulio la Julai, Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya kijeshi ya Ukraine, alisema waasi walipokea "taarifa muhimu walizohitaji" kufanya mashambulizi, ingawa hakutoa ufafanuzi.

Kujibu kauli ya Bw Yusov, Mali iliishutumu Ukraine kwa kukiuka mamlaka yake ya kujitawala na ikatangaza kuwa inavunja uhusiano na Ukraine "mara moja".

Niger ilifuata mkondo huo siku ya Jumanne, huku msemaji wa serikali Amadou Abdramane akitaja matamshi ya Bw Yusov kuwa "hayakubaliki".

Jirani ya Mali Senegal pia ilikemea Ukraine.

Comments
Comment sent successfully!